Upinzani Togo: Tutasitisha maandamano iwapo rais atajiuzulu
Kiongozi wa upinzani nchini Togo amesema maandamano ya wapinzani dhidi ya serikali ya nchi hiyo yataendelea kushuhudiwa madhali Rais Faure Gnassingbe wa nchi hiyo ataendelea kung'ang'ania madaraka.
Jean-Pierre Fabre, mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Togo cha National Alliance for Change ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, lazima Rais Gnassingbe ajiuzulu, la sivyo serikali yake ya kifamilia iliyotawala zaidi ya miongo mitano itaendelea kushuhudia malalamiko na ghadhabu za wananchi.
Hapo jana maelfu ya wananchi wa Togo waliandamana kwa siku ya tatu mfululizo katika mitaa ya mji mkuu wa nchi hiyo wakimtaka Rais Faure Gnassingbe ang'atuke madarakani, hatua ambayo imetajwa kuwa ni changamoto kubwa kwa familia hiyo iliyoko madarakani nchini Togo kwa muda wa miaka hamsini. Faure Gnassingbe amekuwa katika hatamu za uongozi tangu kufariki dunia baba yake mwaka 2005.
Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji ambao walikuwa wakichoma moto tairi za magari katika ngome ya upinzani katika eneo la Be katika mji mkuu wa nchi hiyo, Lome.
Hii ni katika hali ambayo, Mohamed Ibn Chambas, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Togo ameitaka serikali ya nchi hiyo iwatimizie wananchi matarajio waliyonayo wakati polisi wa nchi hiyo wakiripotiwa kukabiliana na waaandamanaji wanaotaka kuhitimishwa utawala wa kifamilia wa miaka hamsini nchini humo huku akisisitiza kuwa anataraji kwamba chama tawala nchini Togo na vyama vya upinzani vitafikia makubaliano.