Mwito wa kutumiwa Kiswahili kuimarisha utangamano Afrika Mashariki
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34111-mwito_wa_kutumiwa_kiswahili_kuimarisha_utangamano_afrika_mashariki
Naibu Waziri Mkuu wa Uganda ametoa wito wa kutumiwa lugha ya Kiswahili kuimarisha utangamano katika kanda ya Afrika Mashariki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 09, 2017 03:19 UTC
  • Mwito wa kutumiwa Kiswahili kuimarisha utangamano Afrika Mashariki

Naibu Waziri Mkuu wa Uganda ametoa wito wa kutumiwa lugha ya Kiswahili kuimarisha utangamano katika kanda ya Afrika Mashariki.

Kirunda Ali Kivejinja ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC wa Uganda amesema ni kupitia utumiaji wa lugha ya Kiswahili tu ambapo kanda ya Afrika Mashariki itafikia kilele cha nukta zilizoainishwa katika Ibara ya 137 (2) ya Mkataba wa Kuundwa EAC.

Kivenjia aliyasema hayo katika hafla ya kufunga Duru ya Kwanza ya Kongamano la kuzindua Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki (EAKC) visiwani Zanzibar lililoanza tarehe Septemba 6 na kumalizika jana Ijumaa.

Kirunda Ali Kivenjia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC amesema: "Jumuiya hii ina azma thabiti ya kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG's) na kwa msingi huo, baraza la EAKC linafaa kuja na mapendekezo ya nafasi na matumizi ya lugha ya Kiswahili katika kufanikisha hayo ."

Bendera za nchi wanachama wa EAC

Naibu Waziri Mkuu wa Uganda amekumbusha kuwa, waasisi wa Tanzania walitambua umuhimu wa kukitumia Kiswahili kama chombo cha utangamano nchini humo na ndiposa uepo wa makabila karibu 120 haujawahi kusababisha au kueneza uozo wa ukabila nchini humo.

Profesa Kenneth Simala, Katibu Mkuu wa Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki kwa upande wake amesema jitihada za kukifanya Kiswahili kiwe lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaendelea na wanatumai karibu hivi zitazaa matunda.

Mapema mwaka huu, uamuzi wa bunge la Rwanda wa kuidhinisha Kiswahili kama lugha rasmi nchini humo kulipokelewa kwa msisimko wa aina yake na Wanyarwada. Rwanda ambayo ni mwanachama wa EAC ilichukua hatua hiyo baada ya hoja hiyo kupokea baraka kamili za Baraza la Mawaziri mwaka jana.