Wanazuoni wa Algeria wapinga kuondolewa "Bismillah" katika vitabu vya shule nchini humo
Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu nchini Algeria imekosoa vikali hatua ya Wizara ya Elimu ya nchi hiyo ya kuondoa neno "Bismillahi Rahman Rahiim" katika vitabu vya mwaka mpya wa masomo nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu wa Algeria imemshambulia vikali Waziri wa Elimu wa nchi hiyo, Nuria Benghabrit Remaoun kwa kuamuru kuondolewa neno Bismillahi Rahman Rahiim kwenye vitabu vya mwaka mpya wa masomo na kuitaja hatua hiyo kuwa ni hujuma dhidi ya akili na hisia za watoto wa Algeria na utambulisho wa kitaifa wa nchi hiyo.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, Waziri wa Elimu, Nuria Benghabrit Remaoun anawalenga watoto wa shule za msingi katika jitihada za kuwalea kwa misingi ya kilaki na kutupilia mbali maadili na mafundisho ya dini.
Neno Bismillahi Rahman Rahiim limekiwa likiandikwa katika ukurasa wa kwanza wa vitabu vyote vya masomo ya shule nchini Algeria tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1962.
Duru za habari nchini Algeria zinasisitiza kuwa, kuondolewa jina la Mwenyezi Mungu na Bismillah Rahmani Rahiim kwenye vitabu vya masomo nchini humo ni sehemu ya vita vya wakoloni wa zamani ambao sasa wanatumia walimu na vituo vya masomo vya Wamagharibi vinavyoanzishwa nchini humo kama mikono ya ukoloni mamboleo.