Kenya yachelewesha kuanza vikao vya EALA tangu Juni 2017
(last modified Fri, 22 Sep 2017 08:04:05 GMT )
Sep 22, 2017 08:04 UTC
  • Kenya yachelewesha kuanza vikao vya EALA tangu Juni 2017

Hatua ya Kenya kutoteua wabunge wake wa Bunge la Afrika Mashariki EALA hadi sasa imechelewesha kuanza vikao vya chombo hicho cha kieneo.

Bobi Odiko, Afisa Mkuu wa Uhusiano Mwema wa EALA ameliambia gazeti la New Times la Rwanda kuwa, Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki walitazamiwa kuapishwa Juni 6 mwaka huu na kuanza vikao vyao mara moja, lakini hilo halijafanyika hadi sasa kwa kuwa Kenya haijateua wanachama wake 9 wa kuiwakilisha katika taasisi hiyo ya kikanda.

Amesema nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC zimekwishawateua Wabunge wao tisa isipokuwa Kenya na kwa msingi huo, vikao vya bunge hilo vitaendelea kuakhirishwa hadi Kenya itakapoteua wanachama wake.

Afisa huyo wa mawasiliano wa EALA amesema bunge hilo la kieneo linasubiriwa na kibarua cha kujadili na kupasisha kuwa sheria, miswada 13, sambamba na kuteua Spika mpya na wakuu wa Kamisheni ya bunge hilo.

Bendera za nchi wanachama wa EAC

Maafisa wa EALA wanasema hatua ya Mahakama ya Juu ya Kenya kubatilisha matokeo ya urais na hata Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Kenya IEBC kuchelewesha uchaguzi wa marudio hakuathiri utenda kazi wa Bunge la Kenya na hivyo lina jukumu la kuchangamkia uteuzi wa wawakilishi wake katika bunge hilo la kikanda.

Wabunge wa Bunge la 12 la Kenya waliapishwa Agosti 31 mwaka huu. Agosti 10, Bunge la Kenya, liliziandikia barua nchi wanachama wa EAC, likisisitiza kuwa uteuzi wa Wabunge 9 wa EALA utapewa kipaumbele mara shughuli za bunge zitakapoanza.

Bunge la 11 la Kenya lilishindwa kufanya uteuzi wa wanachama wa Bunge la Afrika Mashariki, baada ya kambi ya serikali na upinzani bungeni kulumbana kuhusu majina yaliyopendekezwa.

Tags