Umoja wa Mataifa wayataka makundi ya kisiasa Togo kuanza mazungumzo ya maana
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34779-umoja_wa_mataifa_wayataka_makundi_ya_kisiasa_togo_kuanza_mazungumzo_ya_maana
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitolea wito serikali na makundi yote ya kisiasa ya Togo kuanza mazungumzo ya maana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 24, 2017 04:08 UTC
  • Umoja wa Mataifa wayataka makundi ya kisiasa Togo kuanza mazungumzo ya maana

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitolea wito serikali na makundi yote ya kisiasa ya Togo kuanza mazungumzo ya maana.

Antonio Guterres jana alifanya mazungumzo na Komi Selom Klassou Waziri Mkuu wa Togo na kuzitaka serikali na wanaharakati wote wa kisiasa nchini humo kuanza mazungumzo mapana ili kujadili marekebisho muhimu yanayopaswa kufanyika huko Togo. Watu watano waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika maandamano yaliyofanyika mwezi Agosti mwaka huu huko Togo yaliyoitishwa na chama cha Kitaifa cha Pan African. 

Wapinzani wa serikali ya Togo wamekosoa baadhi ya vipengee vya marekebisho ya sheria ya uchaguzi. Rais Faure Gnassingbe wa Togo anaweza kugombea tena kiti cha urais mwaka 2020 na 2025 licha ya kuainishwa muhula wa kuwepo madarakani rais. Wapinzani hao wa Togo wanataka kurejeshwa tena katiba iliyopasishwa mwaka 1992 ambayo inatia ukomo kipindi cha rais kuweko madarakani na pia wanamtaka Rais Faure Gnassingbe aondoke madarakani. 

Rais Faure Gnassingbe wa Togo 

Rais Gnassingbe ameliongoza taifa hilo la Afrika magharibi tangu baba yake afariki dunia mwaka 2005 baada ya kuwa madarakani kwa miaka 38. Mwaka 1992 marehemu Gnassingbe Eyadema alipitisha sheria ambayo rais alipasa kuweko madarakani kwa mihula miwili pekee hata hivyo muongo mmoja baadaye Gnassingbe Eyadema aliifutilia mbali sheria hiyo.