Mazungumzo ya makundi hasimu ya Libya yanaendelea Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34915-mazungumzo_ya_makundi_hasimu_ya_libya_yanaendelea_tunisia
Mazungumzo baina ya makundi hasimu nchini Libya yaliyoanza jana Jumanne katika nchi jirani ya Tunisia yanaendelea chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa kwa lengo la kukomesha mgogoro wa miaka sita wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 27, 2017 06:28 UTC
  • Mazungumzo ya makundi hasimu ya Libya yanaendelea Tunisia

Mazungumzo baina ya makundi hasimu nchini Libya yaliyoanza jana Jumanne katika nchi jirani ya Tunisia yanaendelea chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa kwa lengo la kukomesha mgogoro wa miaka sita wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Mazungumzo hayo yalifunguliwa kwa hotuba ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa, Gassan Salame ambaye amezitaka pande mbili zinazoshiriki katika mazungumzo hayo ziweke pembeni hitilafu zao na kumaliza kazi iliyowapeleka nchini Tunisia katika muda uliopangwa.

Walibya katika mazungumzo ya amani nchini Tunisia

 

Amesema, Walibya wote wameshachoka. Hadi sasa wamekuwa wakitoka kwenye kipindi kimoja cha mpito na kuingia kwenye kipindi kingine cha mpito na mlolongo huo hauna mwisho. Amesema, kuna taasisi zimelala, inabidi ziamshwe. Vile vile kuna taasisi zina mizozo, inabidi ziunganishwe na kuna baadhi ya taasisi zimetekwa nyara, inabidi zijengwe upya.

Mazungumzo hayo yamekuja wiki moja baada ya mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa kutangaza mwaka mmoja wa mpango madhubuti wa kipindi cha mpito cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa rais na bunge nchini Libya.

Hivi sasa kuna mabunge mawili hasimu nchini Libya na wajumbe wa mabunge hayo wako katika mazungumzo nchini Tunisia hivi sasa kuhusiana na namna ya kufanyia marekebisho mpango wa Amani wa Umoja wa Mataifa uliotiwa saini mwaka 2015.