WFP kupunguza chakula wanachopata wakimbizi nchini Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35151-wfp_kupunguza_chakula_wanachopata_wakimbizi_nchini_kenya
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WPF, litapunguza kwa asilimia 30 mgao wa chakula kwa wakimbizi 420,000 walio kwenye kambi za Daadab na Kakuma nchini Kenya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 03, 2017 00:32 UTC
  • WFP kupunguza chakula wanachopata wakimbizi nchini Kenya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WPF, litapunguza kwa asilimia 30 mgao wa chakula kwa wakimbizi 420,000 walio kwenye kambi za Daadab na Kakuma nchini Kenya.

Uamuzi huo umetangazwa na mwakilishi mkazi wa shirika hilo nchini Kenya Bi Annalisa Conte , akisema wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha na hivyo wanahitaji kwa haraka dola milioni 28.5 ili kufikisha msaada wa chakula kwa wakimbizi katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Amesema kutokana na ukata huo kuanzia mwezi huu, WFP itapunguza mgao wa chakula katika kambi hizo

Aidha, WFP haitatoa unga wenye virutubisho  kwa wakimbizi wote kama hapo  awali isipokuwa itawapa kipaumbele wanawake wajawazito na wanawake wanaonyonyesha watoto kupitia kliniki za afya, jambo ambalo amesema litaongeza viwango vya utapiamlo kwa wakimbizi.

WFP imekua ikitoa msaada wa  chakula na posho kwa wakimbizi mwaka huu kutokana na michango kutoka kwa wahisani  kama vile Canada, China, Umoja wa Ulaya, Ujerumani, Hungary, Japan, Sweden, Uingereza na Marekani.

Aghalabu ya wakimbizi katika kambi ya Kakuma ya kaskaizni mwa Kenya ni kutoka Sudan Kusini huku kambi ya Dadaab ya kaskazkini mashariki mwa Kenya ikiwa na wakimbizi kutoka nchi jirani ya Somalia.

Hayo yanajiri baada ya Umoja wa Mataifa kuonya kuwa dunia sasa inakabiliwa na janga kubwa zaidi la wakimbizi tokea Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.