Makomando 3 Wamarekani wauawa nchini Niger
(last modified Thu, 05 Oct 2017 07:48:15 GMT )
Oct 05, 2017 07:48 UTC
  • Makomando 3 Wamarekani wauawa nchini Niger

Makomando watatu wa kikosi maalumu cha jeshi la Marekani wameuawa katika shambulizi la kuvizia nchini Niger wakiwa katika oparesheni ya kutoa mafunzo kwa jeshi la nchi hiyo.

Taarifa zinasema makomando hao ambao ni maarufu kama Green Berets walifyatuliwa risasi na watu wasiojulikana Jumatano ambapo watatu waliuawa na wengine wawili wakajeruhiwa.

Shambulizi hilo la kuvizia linaripotiwa kutekelezwa karibu na mji mkuu wa Niger, Niamey siku ya Jumatano. Maafisa wa usalama katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi wanasema yamkini hujuma hiyo imetekelezwa na  mtandao wa al-Qaeda la eneo la Maghreb barani Afrika maarufu kama AQIM.

Ripoti zinasema wanajeshi watano wa Niger ni kati ya waliouawa katika shambulizi hilo ambalo lilijiri wakati askari hao walikuwa katika doria pamoja na makomando hao Wamarekani karibu na mpaka ya Nigeri na Mali.

Makomando wa Marekani

Maafisa wa Niger wanasema wanaamini waliotekeleza hujuma hiyo waliingia nchini humo kutoka nchi jirani ya Mali.

Mwezi Mei pia makomando wawili wa Marekani waliuawa katika shambulizi la kundi la kigaidi la Al Shabab nchini Somalia.

Maelfu ya wanajeshi wa Marekani wanaripotiwa kuweko katika nchi kadhaa za Kiafrika katika kile kinachoonekana na jitihada za Washington kutumia kisingizo cha ugaidi kueneza satwa yake ya kijeshi barani Afrika.

 

Tags