Watu 100 wameuawa katika machafuko ya hivi karibuni nchini Cameroon
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35299-watu_100_wameuawa_katika_machafuko_ya_hivi_karibuni_nchini_cameroon
Mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu katikati mwa Afrika umetangaza kuwa, jumla ya watu 100 waliuawa katika machafuko yaliyoibuka hivi karibuni katika maeneo mawili ya watu wanaozungumza lugha ya Kingereza nchini Cameroon.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 06, 2017 10:50 UTC
  • Watu 100 wameuawa katika machafuko ya hivi karibuni nchini Cameroon

Mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu katikati mwa Afrika umetangaza kuwa, jumla ya watu 100 waliuawa katika machafuko yaliyoibuka hivi karibuni katika maeneo mawili ya watu wanaozungumza lugha ya Kingereza nchini Cameroon.

Taarifa iliyotolewa na mtandao huo wa watetezi wa haki za binaadamu eneo la katikati mwa Afrika imesema kuwa, watu hao waliuawa kwa kumiminiwa risasi na askari na maafisa usalama wa Cameroon sambamba na kuvuta hewa ya gesi ya kutoa machozi wakati wa kujiri maandamano ya kutaka kujitenga na serikali kuu ya Yaoundé nchini humo.

Vurugu za tarehe Mosi Oktoba nchini Cameroon

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hali ya kaskazini na kusini magharibi mwa Cameroon, sehemu ambazo wakazi wake wanazungumza lugha ya Kingereza, ni ya kutia wasi wasi mkubwa. Kadhalika mtandao huo wa watetezi wa haki za binaadamu katikati mwa Afrika umelaani vikali mienendo ya utumiaji mabavu inayofanywa na baadhi ya maafisa usalama wa nchi hiyo dhidi ya wapinzani. Awali duru rasmi za habari nchini humo zilitangaza kuuawa makumi ya watu waliokuwa wanaandamana dhidi ya serikali.

Askari wa Cameroon wakijaribu kudhibiti hali ya mambo nchini

Malalamiko yaliyoanza tarehe Mosi Oktoba mwaka huu nchini Cameroon na ambayo yaliitishwa kwa lengo la kutaka kujitenga eneo la watu wanaozungumza lugha ya Kingereza (Anglophone) kutoka eneo la watu wanaozungumza lugha ya Kifaransa (Francophone), yalizimwa na askari wa serikali kwa kutumia mtutu wa bunduki. Wakazi wa eneo hilo ambao wanaunda asilimia 20 kati ya jamii yote ya watu milioni 20 ya Cameroon, wanasema kuwa, wamekuwa wakitengwa na serikali kuu ya Yaoundé kiasi cha kuwapelekea kutaka kujitenga na kujitangazia uhuru.