Watu watatu wauawa katika shambulio la kituo cha UN, DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35337-watu_watatu_wauawa_katika_shambulio_la_kituo_cha_un_drc
Watu watatu wameuawa na askari wawili wa Umoja wa Mataifa wamejeruhiwa baada ya kundi la watu kushambulia kituo cha kijeshi cha Umoja wa Mataifa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jana Ijumaa.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 07, 2017 04:21 UTC
  • Watu watatu wauawa katika shambulio la kituo cha UN, DRC

Watu watatu wameuawa na askari wawili wa Umoja wa Mataifa wamejeruhiwa baada ya kundi la watu kushambulia kituo cha kijeshi cha Umoja wa Mataifa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jana Ijumaa.

Jenerali Bernard Commins, msaidizi wa mkuu wa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini humo amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa: "Saa kumi alfajiri, kundi la watu wenye silaha ambao inadhaniwa ni waasi wa Mai-Mai wameshambulia kituo cha MONUSCO (Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa DRC) karibu na katikati ya mkoa wa Lubero."

Bernard Commins msaidizi wa mkuu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani DRC, Monusco

 

"Washambuliaji watatu wameuawa wakati wanajeshi wa Umoja wa Mataifa walipojibu mashambulizi na mwengine mmoja amejeruhiwa na baadaye kuchukuliwa na wanajeshi wa MONUSCO kwa ajili ya kutibiwa," amesema na kuongeza kuwa, "askari wawili wa Kofia Buluu wamejeruhiwa kidogo katika shambulizi hilo."

Mkoa wa Lubero uko umbali wa kilomita 300 kaskazini mwa mji wa Goma, ambao ni makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Machafuko katika maeneo hayo yanaendelea kwa zaidi ya miaka 20 sasa. Baadhi ya wakati mapigano huzuka baina ya makundi hasimu ya waasi na baadhi ya wakati baina ya wanajeshi wa serikali na waasi na wakati mwingine kati ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na makundi ya waasi.