Oct 10, 2017 08:12 UTC
  • Kesi ya mamia ya magaidi wa Boko Haram yaanza kusikilizwa Nigeria

Wizara ya Sheria ya Nigeria imetangaza habari ya kuanza kusikilizwa kesi ya wanachama zaidi ya elfu mbili wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika mahakama mbalimbali za nchi hiyo.

Wizara hiyo imemnukuu Jaji Binta Nyako akisema jana kwamba mchakato wa kusikilizwa kesi za wanachama zaidi ya elfu mbili wa genge la kigaidi la Boko Haram umeanza rasmi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kuna wanachama elfu moja na 670 wa kundi la kigaidi la Boko Haram ambao wanashikiliwa katika kambi ya kijeshi ya Kainji katika jimbo la Niger Delta la magharibi mwa Nigeria. Kesi za za wanachama hao wa Boko Haram zinasikilizwa faragha katika mahakama za kambi hiyo ya kijeshi.

Boko Haram wanafanya uharibifu mkubwa nchini Nigeria

 

Wizara ya Sheria ya Nigeria imeongeza kuwa, wanachama 651 pamoja na mtuhumiwa mwingine mmoja wa ugaidi wanashikiliwa katika kambi ya kijeshi ya Giwa huko Maidiguri, makao makuu ya jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa Nigeria ambalo wakati fulani lilikuwa ngome ya magaidi wa Boko Haram.

Genge la Boko Haram lilianzisha mashambulizi nchini Nigeria mwaka 2009 kwa madai ya kupinga elimu za nchi za Magharibi. Zaidi ya raia 20 elfu wa Nigeria, Cameroon, Niger na Chad wameshapoteza maisha yao kutokana na mashambulizi ya genge hilo la kigaidi tangu wakati huo hadi hivi sasa na wengine zaidi ya milioni mbili wamekuwa wakimbizi.

Tags