Odinga ajitoa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa marudio wa rais wa Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35485-odinga_ajitoa_kwenye_kinyang'anyiro_cha_uchaguzi_wa_marudio_wa_rais_wa_kenya
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametangaza leo kuwa hatogombea katika uchaguzi wa marudio wa rais ulioamriwa kuitishwa tena na Mahakama ya Juu ya nchi hiyo ambao umepangwa kufanyika tarehe 26 Oktoba akisema kwamba uchaguzi huo hautokuwa huru na wa haki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 10, 2017 13:21 UTC
  • Odinga ajitoa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa marudio wa rais wa Kenya

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametangaza leo kuwa hatogombea katika uchaguzi wa marudio wa rais ulioamriwa kuitishwa tena na Mahakama ya Juu ya nchi hiyo ambao umepangwa kufanyika tarehe 26 Oktoba akisema kwamba uchaguzi huo hautokuwa huru na wa haki.

Odinga aidha amesema mgombea wake mwenza Kalonzo Musyoka naye pia hatoshiriki kwenye uchaguzi huo.

Amefafanua kuwa muungano wa upinzani wa NASA umefikia hitimisho kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC haina nia ya kuhakikisha ukiukaji wa taratibu na sheria za uchaguzi uliofanywa na tume hiyo katika uchaguzi uliopita hautokei tena.

Amebainisha kwamba ishara zote zilizopo zinaonyesha kuwa uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 26 utakuwa mbovu zaidi kuliko uliotangulia.

Raila Odinga

Mgombea huyo wa urais kwa tiketi ya muungano wa upinzani wa NASA amekikosoa pia chama tawala cha Rais Uhuru Kenyatta cha Jubilee kwa kutaka kuzifanyia marekebisho sheria za uchaguzi na kueleza kwamba hatua hiyo inaonyesha kuwa chama hicho hakitaki kuwepo ushindani katika mazingira ya usawa. Ameongeza kuwa inachotaka serikali ya Jubilee ni kuona lazima inashinda uchaguzi hata kama kwa kuvunja sheria.

Odinga ametangaza msimamo huo katika hali ambayo Rais Uhuru Kenyatta amesisitiza kuwa uchaguzi huo wa marudio utafanyika kama ilivyopangwa licha ya mshindani wake kujitoa.

Rais Uhuru Kenyatta

Nayo tume ya uchaguzi IEBC imetangaza kuwa kufuatia uamuzi wa Odinga kujitoa kwenye uchaguzi, tume hiyo na timu yake ya wanasheria watakutana kujadili hatua za kuchukua.

Mara baada ya Odinga kutangaza uamuzi wa kujitoa kwenye uchaguzi wa marudio, Seneta James Orengo, mmoja wa watu wa karibu wa mgombea huyo wa urais kwa tiketi ya NASA ametoa wito wa kufanyika maandamano ya upinzani ya nchi nzima.

Orengo amesema maandamano ya nchi nzima yatafanyika hapo kesho kwa msingi kwamba kama hakuna marekebisho hakutokuwa na uchaguzi.../