Watu 3 wauawa katika maandamano ya wapinzani nchini Kenya
Watu watatu wameripotiwa kuuawa katika maandamano ya wapinzani nchini Kenya ambao wanataka mabadiliko katika Tume Huru ya Uchaguzi IEBC.
Taarifa zinasema watu hao wameuawa katika maandamano ambayo yaligeuka kuwa ghasia katika Kaunti ya Siaya katika eneo la Nyanza ambayo ni ngome ya kinara wa muungano wa upinzani, NASA, Raila Odinga.
Gazeti la Daily Nation limeripoti kuwa watu hao watatu wameripotiwa kupigwa risasi wakati walipojaribu kuvamia kituo cha polisi katika mji wa Bondo anakotoka Odinga.
Katika miji wa Homa Bay, Kisumu na Migori ambayo yote ni ya eneo la Nyanza pia watu kadhaa wamejeruhiwa katika makabiliano na maafisa wa polisi.
Maandamano pia yameripotiwa katika mji mkuu, Nairobi huku kukiwa pia na mijimuiko ya kupinga tume ya uchaguzi mjini Mombasa. Waandamanaji katika miji ya Nairobi, Mombasa na Kisumu wamepuuza agizo la kaimu waziri wa usalama Bw. Fred Matiang’i ambaye jana alipiga marufuku mijumuiko katikati ya miji hiyo. Waandamanaji wanataka mabadiliko katika tume ya uchaguzi hasa kutimuliwa afisa mkuu mtendaji Ezra Chiloba. Hayo yanajiri katika hali ambayo kinara wa upinzani Raila Odinga ameshajiondoa katika uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 na hivi sasa yuko mjini London Uingereza kuhutubia vikao mbali mbali.