Watu 3 wauawa katika ghasia zilizozuka baada ya imam kukamatwa Togo
Kwa akali watu watatu wameuawa kwenye ghasia katika mji wa Sokode kaskazini mwa Togo, baada ya imam wa msikiti mmoja katika eneo hilo kukamatwa na maafisa wa polisi.
Aime Adi, mwakilishi wa Amnesty International nchini humo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, machafuko hayo yaliyozuka usiku wa kuamkia leo, yalianza baada ya maafisa usalama kumkamata Alpha Alassane, imam mashuhuri katika mji huo anayetajwa kuwa na uhusiano wa karibu na viongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Pan African (PNP).
Amesema walinzi wawili wa nyumba ya afisa mmoja mwandamizi serikalini na fundi seremala wameuawa katika ghasia hizo za jana usiku.
Kanali Yark Damehame, Waziri wa Usalama wa Togo amesema serikali imelazimika kumtia mbaroni imam huyo kwa kuwa amekuwa akitoa hotuba za kichochezi dhidi ya serikali.
Wafuasi wa chama hicho cha upinzani wametishia kufanya maandamano kesho Jumatano na Alkhamisi iwapo Alpha Alassane ataendelea kuzuiliwa na vyombo vya usalama.
Itakumbukwa kuwa, watu watano waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika maandamano yaliyofanyika mwezi Agosti mwaka huu huko Togo yaliyoitishwa na chama cha PNP.
Wapinzani hao wa Togo wanataka kurejeshwa tena katiba iliyopasishwa mwaka 1992 ambayo inatia ukomo kipindi cha rais kuweko madarakani huku wakimtaka Rais Faure Gnassingbe wa nchi hiyo aondoke madarakani.