Ghasia zashtadi Uganda, Besigye na Wabunge wa upinzani wakamatwa
Mtu mmoja ameuawa huku wengine sita wakiachwa na majeraha ya risasi na kulazwa hospitalini katika wilaya ya Rukungiri, kufuatia ghasia zilizotokana na maandamano ya kupinga mpango wa kuondoa kikomo cha umri wa kugombea urais nchini Uganda.
Inaarifiwa kuwa maafisa wa polisi walitumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi na risasi za plastiki na risasi hai kuwatawanya waandamanaji katika mji wa Nyakibale.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor, jana jioni kinara wa upinzani nchini Uganda Dakta Kizza Besigye pamoja na maafisa wengine wawili wa ngazi za juu wa chama cha FDC walikamatwa na maafisa wa polisi katika kijiji cha Burambira wakielekea wilaya ya Kabale.
Kamanda Mkuu wa Polisi katika eneo hilo Denis Namuwoza amesema Besigye na wenzake wamekamatwa kwa tuhuma za kujaribu kuua mafisa wa polisi sambamba na kufanya mkutano uliopigwa marufuku. Jeshi la polisi nchini Uganda Jumatano iliyopita lilipiga marufuku kile lilichokiita ni maandamano haramu ya kupinga mpango wa kuondoa kipengee cha umri wa kugombea urais.
Mapema jana polisi ya Uganda iliwatia mbaroni pia Kato Lubwama, Mbunge wa Rubaga Kusini na mwenzake wa Butambala Muwanga Kivumbi kwa kuongoza maandamano ya kupinga juhudi za kuondoa kipengee cha Katiba kilichoweka kikomo cha umri wa kugombea urais, hatua ambayo wapinzani wanaitizama kama mpango wa kumfungulia njia Rais Yoweri Museveni kuendelea kubakia madarakani.
Museveni mwenye umri wa miaka 73, ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu, kisheria hafai kuwania tena urais katika uchaguzi mkuu wa 2021 kwa sababu katiba ya Uganda imeainisha miaka 75 kuwa kikomo cha umri wa mtu anayetaka kugombea urais.