Wanajeshi watatu wa Minusma wauawa nchini Mali
Askari jeshi watatu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Mali wameaga dunia baada ya bomu la kutegwa ardhini kulipuka na wengine wawili wamejeruhiwa.
Kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa kilichoko Mali (MINUSMA) kimeeleza kuwa, gari lililokuwa limewabeba wanajeshi wake likisindikiza msafara wa misaada ya kilojistiki katika maeneo ya Tessalit na Aguelhok kaskazini mwa Mali lilikanya bomu la kutegwa ardhini na kulipuka. Uraia wa wanajeshi hao walioaga dunia bado haujatangazwa.
Askari jeshi wa kulinda amani wa kikosi cha MINUSMA zaidi ya 80 wameuawa tangu mwaka 2013 hadi sasa kufuatia mashambulizi ya makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati zao kaskazini na katikati mwa Mali.
Kudhihiri makundi ya kigaidi kama Daesh (ISIS) na al Qaida katika eneo la Sahel barani Afrika kumeyatia wasiwasi madola ya Magharibi khususan Ufaransa ambayo ina maelfu ya wanajeshi katika eneo hilo.
Eneo la Sahel linaundwa na maeneo ya kuanzia magharibi hadi masharki yaani eneo la kaskazini mwa Senegal, kusini mwa Mauritania, katikati mwa Mali, kusini mwa Algeria na Niger, katikati mwa Chad, kusini mwa Sudan, kaskazini mwa Sudan Kusini na Eritrea.