Kaburi la umati lenye makumi ya maiti lagunduliwa Libya
Kaburi la umati lenye miili ya watu wasiopungua 37 limegunduliwa katika viunga vya mji wa Benghazi nchini Libya.
Maiti zilizogunduliwa katika kaburi hilo zimefungwa mikono kwa kamba na zina alama za kupigwa risasi.
Kaburi hilo limegunduliwa katika eneo lisilokuwa na makazi ya watu katika kitongoji cha Abyar kinachodhibitiwa na wapiganaji wa Jenerali mstaafu Khalifa Haftar.
Baadhi ya ripoti zinasema miili iliyokutwa katika kaburi hilo ni ya askari waliokuwa wakishikiliwa katika jela inayodhibitiwa na jeshi la Haftar tangu miezi kadhaa ilkiyopita.
Libya inasumbuliwa na machafuko makubwa ya kisiasa na kiusalama yaliyoanza baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.
Kwa sasa nchi hiyo inatawaliwa na serikali mbili hasimu zinazodhibiti maeneo tofauti.