Ouyahia: Jeshi linafanya njama za kuipindua serikali ya Algeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36160-ouyahia_jeshi_linafanya_njama_za_kuipindua_serikali_ya_algeria
Waziri Mkuu wa Algeria ametahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea mapinduzi ya kijeshi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 04, 2017 11:23 UTC
  • Ouyahia: Jeshi linafanya njama za kuipindua serikali ya Algeria

Waziri Mkuu wa Algeria ametahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea mapinduzi ya kijeshi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Televisheni ya al Hadath imemnukuu Ahmed Ouyahia akisema kwamba wapinzani wa Rais Abdelaziz Bouteflika wanapanga njama za kufanya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali yake.

Hata hivyo Waziri Mkuu huyo wa Algeria amesema kuwa, huu si wakati tena wa mapinduzi ya kijeshi na yeyote anayetaka kuingia madarakani hana budi kutumia masanduku ya kura za wananchi kufanikisha lengo lake hilo.

Rais Abdulaziz Bouteflika wa Algeria

 

Wapinzani wa serikali ya hivi sasa wanamtuhumu Rais Bouteflika kuwa anafanya njama za kugombea tena urais kwa mara ya tano na kubakia madarakani milele nchini Algeria.

Wapinzani hao wamesisitiza kuwa, hali ya kiafya ya Buoteflika ni mbaya sana na hali ilivyo Algeria hivi sasa hairuhusu hata kufikiria tu kwamba atagombea tena urais.

Rais Abdulaziz Bouteflika amekuwa madarakani nchini Algeria tangu mwaka 1999 na mwaka 2008 aliifanyia mabadiliko katiba ya nchi hiyo na kufuta kipengee kilichomzuia kugombea urais kwa zaidi ya vipindi viwili.

Hata hivyo mwaka 2013 alikumbwa na shinikizo la ubongo na tangu wakati huo hadi hivi sasa anaonekana mara chache sana hadharani na katika sherehe za kitaifa.