Nov 06, 2017 02:46 UTC
  • Angola yawatimua maelfu ya wahamiaji haramu wa Kongo DR

Serikali ya Angola imewafukuza nchini humo maelfu ya wahamiaji haramu raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Shirika rasmi la habari la Angola ANGOP limeripoti habari hizo na kuongeza kuwa, wahajiri hao haramu wapatao 2,884 walikamatwa katika mkoa wa Lunda Norte, mpakani mwa nchi mbili hizo, kati ya mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu.

Mkuu wa Polisi katika mkoa huo, Rodrigues Zeca ameliambia shirika hilo la habari kuwa, katika operesheni hiyo ya maafisa usalama mkoani hapo,  Wakongomani wengine 10,128 waliamua kurejea nchini kwao kwa hiari.

Amesema aghalabu ya wahamiaji hao haramu huingia nchini Angola kwa ajili ya kutafuta madini hususan ya almasi katika mikoa ya Lunda Norte na Lunda. Sul

Baadhi ya wahamiaji haramu wa Kongo nchini Angola

Siku chache zilizopita, Angola iliwatimua wahajiri haramu 432 wakiwemo raia wa DRC, waliokamatwa katika mkoa wa Cabinda.

Umoja wa Mataifa hivi karibuni ulitangaza kuwa, mapigano makali kati ya askari wa serikali ya Kongo DR na wanamgambo wa kundi moja la kikabila katika mkoa wa Kasai yamewalazimisha watu zaidi ya milioni moja kuyaacha makazi yao na kwenda kuomba hifadhi katika nchi jirani hasa Angola.

Tags