UN: Kitendo cha EU kuisaidia Libya kuwazuilia wakimbizi sio cha kibinadamu
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema sera ya Umoja wa Ulaya ya kuwasaidia maafisa wa serikali ya Libya kuwazuilia wakimbizi wanaotaka kwenda Ulaya kupitia safari hatari za baharini ni kitendo kisicho cha ubinadamu.
Katika taarifa, Zeid Ra’ad al-Hussein amesema mateso na hali ngumu wanayoshuhudia wakimbizi hao nchini Libya kwa msaada wa EU ni jambo la fedheha kwa ubinadamu.
Amekosoa hatua ya jamii ya kimataifa kuendelea kuifumbia macho kadhia ya wakimbizi hususa wa Kiafrika, wanaopitia kipindi kigumu nchini Libya.
Hata hivyo msemaji wa EU amesema ingawaje hali ya wakimbizi hao wanaozuiliwa Libya ni ya kutisha na isiyokubalika, lakini amesisitiza kuwa Brussels inafadhili mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayofanya operesheni za kuwalinda wakimbizi hao na sio vinginevyo.
Haya yanajiri siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kuanza zoezi la kuwahamisha makumi ya wakimbizi wa nchi za Afrika walioko Libya na kuwapeleka nchini Niger, ili kunusuru maisha yao. Aghalabu yao ni raia kutoka nchi za Eritrean, Ethiopian na Sudan.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, raia wa Kiafrika wapatao 152,000 wamehatarisha maisha yao katika safari hatari za kuelekea barani Ulaya kutafua ajira na maisha kupitia bahari ya Mediterranean, ambapo zaidi ya elfu tatu miongoni mwao wamepoteza maisha hadi sasa.