Umoja wa Afrika waanzisha uchunguzi kuhusu biashara ya utumwa nchini Libya
Umoja wa Afrikka umetangaza kuwa, unaanzisha uchunguzi kuhusiana na ripoti ziliozenea kwamba, wahajiri wa Kiafrika nchini Libya wamekuwa wakiuzwa na kununuliwa kama bidhaa.
Moussa Faki Mahamat, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amewaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya umoja huo mjini Addis Ababa Ethiopia kwamba, AU inaanzisha uchunguzi kuhusiana na kuweko biashara ya utumwa nchini Libya.
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema kuwa, katika uchunguzi huo, taasisi hiyo itahakikisha kwamba, inavifikia vituo ambavyo wahajiri wanashikiliwa kinyume cha sheria nchini Libya ambapo inasemekana kuwa, maelfu ya wahajiri wamekuwa wakishikiliwa bila ya kuelezwa makosa yao.
Aidha Moussa Faki Mahamat ameitaka serikali ya Libya kutoa ushirikiano unaotakiwa katika uchunguzi huo. Kadhalika Umoja wa Afrika umezitaka nchi wanachama wa umoja huo, kusaidia kurejeshwa makwao wahajiri wanaoshikiliwa huko nchini Libya.
Hatua hiyo ya Umoja wa Afrika inafuatia kuenea kwa taarifa za kufanyika biashara ya utumwa nchini Libya ambapo inaelezwa kuwa wahajiri wa Kiafrika wamekuwa wakiuzwa hadharani kama bidhaa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Siku chache zilizopita baadhi ya televisheni zilionyesha mkanda wa video unaoonyesha kufanyika mnada wa wahajiri wa Kiafrika ambapo wahajiri hao walikuwa wakiuzwa na kununuliwa kama bidhaa.
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitaja habari hiyo ya kuuzwa na kununuliwa wahajiri wa Kiafrika nchini Libya kwamba ni ya kutisha mno.