Wawakilishi wa Zakzaky wakataa kuhudhuria mahakamani Nigeria
Timu ya wanasheria wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imechukua uamuzi wa kutohudhuria vikao vya kesi ya kiongozi wa harakati hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky baada ya viongozi wa Nigeria kuwazuia wanachama wa timu hiyo kukutana na mteja wao anayeshikiliwa katika korokoro za nchi hiyo.
Mawakilishi hao wamesema hatua ya serikali ya Nigeria ya kuwazuia kukutana na Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa na jeshi inakiuka maadili na taratibi za kikazi.
Kiongozi wa Harakati ya Waislamu nchini Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky alitiwa nguvuni miezi minne iliyopita baada ya jeshi la nchi hiyo kushambulia makazi yake na kituo cha kidini cha Baqiyatullah katika mji wa Zaria na kuua mamia ya Waislamu. Sheikh Zakyazy aliyejeruhwia kwa kupigwa risasi nne katika mashambulizi hayo anashikiliwa mahala pasipojulikana na makumi ya wenzake.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linasema Waislamu wasiopungua 300 waliuawa katika mashambulizi hayo japokuwa harakati ya Kiislamu ya Nigeria inasema zaidi ya watu 1000 waliuawa shahidi.
Wakati huo huo Kamisheni ya Haki za Binamu ya Kiislamu ya Uingereza (IHRC) imesema faili la mashambulizi na mauaji yaliyofanywa na jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu wa mji wa Zaria limepelekwa Hague katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, uhalifu uliofanywa na jeshi la Nigeria katika kipindi cha tarehe 12 hadi 14 Disemba katika mji wa Zaria dhidi ya Waislamu ni jinai dhidi ya binadamu na kuna udharura wa kutolewa amri ya uchunguzi wa mahakama ya ICC kuhusu uhalifu huo.