Wanajeshi 10 wa Sudan wauawa katika mapigano huko Darfur
(last modified Tue, 28 Nov 2017 07:47:44 GMT )
Nov 28, 2017 07:47 UTC
  • Wanajeshi 10 wa Sudan wauawa katika mapigano huko Darfur

Askari 10 akiwemo kamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Sudan wameuawa katika mapigano mapya yaliyozuka hivi karibuni katika jimbo la Darfur.

Waziri wa Ulinzi wa Sudan, Ali Mohamed Salem amenukuliwa na shirika rasmi la habari la serikali SUNA akisema kuwa, wanajeshi hao waliuawa baada ya gari lao kutekwa na kundi moja la waasi, katika wimbi jipya ya mapigano lilioanza Jumapili iliyopita.

Haya yanajiri masaa machache baada ya kikosi kimoja cha jeshi la Sudan kumtia nguvuni Musa Helal, kamanda wa kundi la waasi wa Darfur katika mkoa wa Darfur Kaskazini kwa tuhuma za kuvunja haki za binadamu.

Wanajeshi wa UNAMID eneo la Darfur

Tangu mwaka 2003, jimbo la Darfur limekumbwa na machafuko na mapigano ya silaha huku makabila ya eneo hilo yakilalamika kuwa serikali imewabagua. 

Machafuko hayo yameshapelekea watu laki tatu kuuawa na karibu milioni mbili na nusu kuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan.

Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa zinaendesha operesheni ya kulinda amani katika jimbo hilo chini ya mwavuli wa kikosi cha UNAMID.