Baraza la Usalama lataka kukomeshwa magendo ya binadamu Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36965-baraza_la_usalama_lataka_kukomeshwa_magendo_ya_binadamu_afrika
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa kuendeshwa vita dhidi ya magendo ya binadamu na biashara ya utumwa katika bara la Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 29, 2017 12:56 UTC
  • Baraza la Usalama lataka kukomeshwa magendo ya binadamu Afrika

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa kuendeshwa vita dhidi ya magendo ya binadamu na biashara ya utumwa katika bara la Afrika.

Nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zilikutana katika kikao cha dharura hapo jana na kusisitizia haja ya kuweko mapambano dhidi ya magendo ya binadamu na kung'olewa mizizi ya biashara ya utumwa barani Afrika.

Kikao hicho kilichoitishwa kwa pendekezo la Ufaransa kilijadili na kuchunguza suala la magendo ya binadamu na kuuzwa kama bidhaa wahajiri wa Kiafrika katika nchi ya Libya na kusisitizia udharura wa kuheshimiwa haki za wakimbizi.

Moja ya vikao vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Aidha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetaka kuweko vita vya kweli dhidi ya magendio na biashara ya binadamu na wakati huo huo kuongezwa uungaji mkono kwa serikali ya Libya ili iweze kukabiliana na changamoto ilizo nazo.

Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amesema katika kikao hicho kwamba,  kuna haja ya kukabiliana na biashara ya utumwa na vitendo vingine vya ukiukaji wa haki za binadamu vinavyofanywa dhidi ya wahajiri wanaopitia Libya wakiwa na nia ya kuelekea barani Ulaya kutafuta maisha mazuri.

Itakumbukwa kuwa, wiki iliyopita, televisheni ya CNN ilirusha hewani mubashara mnada wa kuuza Waafrika huko nchini Libya ambapo kila mtu alikuwa akiuzwa kwa dola zisizopungua 400 za Kimarekani.