'Watumwa' wananyofolewa viungo vya mwili Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37151-'watumwa'_wananyofolewa_viungo_vya_mwili_libya
Imebainika kuwa, baadhi ya raia wa Kiafrika wanaopigwa mnada katika magendo ya binadamu nchini Libya wananyofolewa viungo vyao vya mwili na kuuzwa.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 03, 2017 23:41 UTC
  • 'Watumwa' wananyofolewa viungo vya mwili Libya

Imebainika kuwa, baadhi ya raia wa Kiafrika wanaopigwa mnada katika magendo ya binadamu nchini Libya wananyofolewa viungo vyao vya mwili na kuuzwa.

Wakili na mwanaharakati mashuhuri Bobby Banson amenukuliwa na tovuti ya habari ya GhanaWeb akisema kuwa, binafsi ameshuhudia kanda ya video inayoonyesha mmoja wa 'watumwa' hao akieleza jinsi viungo vya mwili vya mwenzake vilivyong'olewa na kuuzwa.

Amebainisha kuwa: "Ukweli wa mambo ni kuwa, baadhi ya raia hao wa Afrika hawauzwi kwa ajili ya kwenda kufanya kazi Ulaya, bali kwa ajili ya biashara ya viungo vya binadamu kama maini na mapafu."

Wakili huyo na mtetezi wa haki za binadamu ameongeza kuwa, wahajiri hao waliojikuta kwenye mtego wa magendo ya binadamu wanapewa dawa za kulala na kisha viungo vyao vinachukuliwa."

Wahajiri wa Afrika wanaouzwa kama bidhaa nchini Libya

Hivi karibuni, televisheni ya CNN ilirusha hewani mubashara mnada wa kuuza Waafrika huko nchini Libya ambapo kila mtu alikuwa akiuzwa kwa dola zisizopungua 400 za Kimarekani.

Duru mbalimbali za kimataifa, ukiwemo Umoja wa Afrika na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimekosoa vikali biashara hiyo ya utumwa mambo leo inayofanyika nchini Libya.