Israel yaiuzia Sudan Kusini ndege zisizo na rubani
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeiuzia Sudan Kusini ndege zisizo na rubani na kamera za kisasa za usalama zilizogharimu mamilioni ya dola, licha ya nchi hiyo changa zaidi barani Afrika kusumbuliwa na ukosefu wa usalama, machafuko, njaa na wimbi la wakimbizi.
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amesema mpango huo wa kununua 'drones' mbili na kamera 11 za kiusalama kutoka shirika la Kizayuni la Global Group katika hatua ya kwanza, unapania kuimarisha usalama katika mji mkuu, Juba.
Edward Dimitiri, Mkurugenzi wa Masuala ya Teknolijia katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Sudan Kusini amesema licha ya nchi hiyo kukabiliwa na changamoto za kiuchumi, lakini imelazimika kutumia 'mamilioni ya dola' kuimarisha usalama wake hususan katika viwanja vya ndege mjini Juba.
Kfir Shilder, Mkurugenzi wa shirika la Kizayuni la Global Group amesema Israel itaiuzia Sudan Kusini drones zaidi na kamera 100 za usalama katika siku zijazo, na kwamba kamera za kwanza zitatundikwa katika Ikulu ya Rais na Uwanja wa Ndege wa Juba.
Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 baada ya miaka mingi ya vita vya ndani na mwaka 2013 ilitumbukia tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya jeshi linalomuunga mkono Rais Salva Kiir na wafuasi wa aliyekuwa makamu wake, Riek Machar.
Mbali na maelfu ya watu kuuawa, mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.