Umoja wa Afrika kuwarejesha wahajiri 20,000 kutoka Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37309-umoja_wa_afrika_kuwarejesha_wahajiri_20_000_kutoka_libya
Umoja wa Afrika umetangaza kuwa, umepanga kuwarejesha makwao wahajiri elfu ishirini kutoka Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 07, 2017 11:45 UTC
  • Umoja wa Afrika kuwarejesha wahajiri 20,000 kutoka Libya

Umoja wa Afrika umetangaza kuwa, umepanga kuwarejesha makwao wahajiri elfu ishirini kutoka Libya.

Taarifa ya Umoja wa Afrika imeeleza kuwa, kipaumbele cha kwanza ni kuwarejesha wahajiri elfu 20 katika kipindi cha wiki sita ambao kwa sasa wapo katika vituo mbali mbali huko Libya na ambao wako tayari kurejea makwao.

Kabla ya hapo, Umoja wa Afrika ulikuwa umetangaza kuwa, unakusudia kuwarejesha makwao wahajiri elfu kumi na tano kutoka Libya hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Aidha Umoja wa Afrika umetangaza kuwa, baadhi ya nchi za bara hilo tayari zimeanza mchakato wa kuwarejesha makwao raia wao walioko nchini Libya.

Wahajiri wa Kiafrika wakiwa nchini Libya

Hivi karibuni, televisheni ya CNN ilirusha hewani mubashara mnada wa kuuza Waafrika huko nchini Libya ambapo kila mtu alikuwa akiuzwa kwa dola zisizopungua 400 za Kimarekani.

Duru mbalimbali za kimataifa, ukiwemo Umoja wa Afrika na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimekosoa vikali biashara hiyo ya utumwa mambo leo inayofanyika nchini Libya.

Baadhi ya ripoti zimefichua kwamba,  baadhi ya raia wa Kiafrika wanaopigwa mnada katika magendo ya binadamu nchini Libya wananyofolewa viungo vyao vya mwili na kuuzwa.

Hivi karibuni watu wasiopungua 40 walitiwa mbaroni kwa tuhuma za kufanya magendo ya binadamu katika eneo la magharibi mwa Afrika baada ya kusambaa mkanda wa video unaoonesha wakimbizi wa Kiafrika wakipigwa mnada na kuuzwa kama bidhaa nchini Libya.