Wahamiaji 190 waokolewa katika fukwe za Libya
Kikosi cha gadi ya ufukweni cha nchini Libya kimeliokoa kundi la wahamiaji wa Kiafrika ambao walikuwa katika juhudi za kukimbilia barani Ulaya kupitia bahari ya Mediterranean.
Televisheni ya Press TV imemnukuu afisa wa gadi ya ufukweni ya Libya akithibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, katika operesheni hiyo, wahamiaji 190 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wameokolewa katika fukwe za Tripoli, mji mkuu wa Libya wakiwemo wanawake na watoto wadogo.
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema kuwa, zaidi ya wahamiaji laki moja na 60 wamefanikiwa kuingia barani Ulaya mwaka huu kwa kutumia bahari ya Mediterranean.
Libya ndiyo nchi inayotumiwa sana na wahamiaji wa Kiafrika wanaokimbilia maisha bora barani Ulaya.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu 2017 hadi hivi sasa, karibu wahamiaji elfu tatu wameshakufa maji katika bahari ya Mediterranean na kesi nyingi zimetokea wakati wahamiaji hao walipokuwa wanatokeo Libya kuelekea nchini Italia kwa kutumia bodi dhaifu sana ambazo zinakuwa rahisi kupinduka.