Liberia yatangaza tarehe ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37551-liberia_yatangaza_tarehe_ya_duru_ya_pili_ya_uchaguzi_wa_urais
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Liberia imetangaza Disemba 26 kuwa tarehe ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 13, 2017 11:43 UTC
  • Liberia yatangaza tarehe ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Liberia imetangaza Disemba 26 kuwa tarehe ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Jerome Korkoya amewataka wananchi waliotimiza masharti ya kupiga kura kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo.

Amesema, na hapa tunanukuu: "Tunawaomba wapiga kura wajitoe mhanga kushiriki zoezi hili la kidemokrasia siku moja baada ya Krismasi, kwa maslahi ya taifa."

Hatua hii inajiri baada ya Mahakama Kuu ya Liberia hivi karibuni kutupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa duru ya kwanza na kusema kuwa, ushahidi wa vitendo visivyokubalika katika uchaguzi huo uliofanyika mwezi Oktoba hautoshi kubatilisha matokeo yake na kuufanya urudiwe.

Rais  Ellen Johnson Sirleaf  wa Liberia

Kwa mujibu wa katiba na sheria ya uchaguzi nchini humo, sharti mgombea wa urais apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zote halali zilizopigwa ili atangazwe mshindi wa urais.

Awali duru ya pili ya kumchagua mrithi wa Rais  Ellen Johnson Sirleaf ilikuwa imepangwa kufanyika mwezi uliopita wa Novemba, lakini kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa duru ya kwanza ilivuruga ratiba ya Tume ya Uchaguzi.

Sirleaf ambaye ni Rais wa kwanza mwanamke kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia nchini humo na pia mshindi wa Tuzo ya Nobel, aliingia madarakani mwaka 2006, baada ya mtangulizi wake, Charles Taylor, kuondolewa madarakani kwa nguvu na waasi mwaka 2003.