Wahajiri karibu 200 waokolewa katika pwani ya Libya
Kikosi cha Jeshi la Majini la Libya kimeokoa wahajiri karibu 200 katika pwani ya magharibi mwa nchi hiyo katika Bahari ya Mediterania waliokuwa wakielekea Ulaya.
Kikosi cha Jeshi la Majini la Libya leo Ijumaa kilitangaza kuwa wahamiaji haramu 195 wakiwemo wanawake 21 na watoto 2 kutoka nchi mbalimbali barani Afrika wameokolewa katika pwani ya magharibi mwa mji wa Garrabulli eneo ambalo kunafanyika biashara haramu ya wahajiri huko kaskazini mwa Afrika.
Jeshi la Majini la Libya Jumatano wiki hii pia liliwaokoa wahajiri 114 katika pwani ya kitongoji cha Garrabulli. Hayo yameelezwa na Idara ya Kupambana na Wahamiaji Haramu ya Libya.
Libya imekuwa ikitumiwa kama nukta ya kuanzia safari za wakimbizi na wahajiri vijana wa Kiafrika kuelekea Ulaya.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2017 hadi sasa karibu wakimbizi elfu tatu wameaga dunia wakijaribu kufika Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania, vifo ambavyo vingi vimetokea katika njia ya bahari kutoka Libya kuelekea Italia.