Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa atembelea Libya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian ameyataka makundi hasimu nchini Libya kuheshimu juhudi za upatanishi za Umoja wa Mataifa na kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2018
Nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika hivi sasa ina serikali mbili hasimu, moja iko mashariki na nyingine ni ile iliyoko magharibi mwa Libya makao makuu yake yakiwa ni mji mkuu Tripoli na ambayo inatambuliwa kimataifa.
Ufaransa ilikuwa mstari wa mbele katika uvamizi wa kijeshi wa NATO na ilituma ndege zake mara kwa mara kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo tofauti ya Libya katika kampeni ya kumpindua Kanali Muammar Gaddafi.
Umoja wa Mataifa ulianzisha duru mpya ya mazungumzo mwezi Septemba nchini Tunisia kati ya makundi hasimu ya Libya kwa nia ya kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi wa rais na bunge mwakani. Hata hivyo mazungumzo hayo yalivunjika mwezi mmoja baadaye kabla ya kufikia natija.
Mara baada ya kuwasili mjini Tripoli na kuonana na waziri mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa, Fayez Sarraj, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa amesema, ameona hamu ya Fayez Sarraj ya kuheshimu mpango huo wa Umoja wa Mataifa wa kuitisha uchaguzi wa rais na bunge.
Baada ya hapo Le Drian ameelekea mjini Benghazi na kuonana na kamanda wa kijeshi mwenye nguvu Khalifa Haftar ambaye siku ya Jumapili alisema kuwa serikali ya Tripoli na mpango wa Umoja wa Mataifa vimepitwa na wakati.
Haftar ni maarufu kati ya wananchi wa upande wa mashariki mwa Libya, lakini ana wapinzani wengi upande wa magharibi mwa nchi hiyo.