Makumi ya Wanyarwanda wafunguliwa mashitaka ya ugaidi Uganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38251-makumi_ya_wanyarwanda_wafunguliwa_mashitaka_ya_ugaidi_uganda
Habari kutoka Kampala, mji mkuu wa Uganda zinasema raia 45 wa Rwanda wanaozuiliwa katika kituo cha polisi cha Nalufenya wilayani Jinja wamefunguliwa mashitaka ya ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 29, 2017 04:35 UTC
  • Makumi ya Wanyarwanda wafunguliwa mashitaka ya ugaidi Uganda

Habari kutoka Kampala, mji mkuu wa Uganda zinasema raia 45 wa Rwanda wanaozuiliwa katika kituo cha polisi cha Nalufenya wilayani Jinja wamefunguliwa mashitaka ya ugaidi.

Wanyarwanda hao walikamatwa wiki mbili zilizopita katika eneo la Kikagati, wilaya ya Isingiro katika mpaka wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki na Tanzania.

Msemaji wa Polisi ya Uganda, Emilian Kayima amesema raia hao wa Rwanda walikamatwa wakiwa wamebeba stakabadhi na vitambulisho ghushi.

Amesema kama tunavyomnukuu: "43 miongoni mwao walikamatwa wakijaribu kutoroka nchi wakiwa na vyeti na vitambulisho bandia. Wawili walikamatwa mjini Kampala na baada ya usaili na uchunguzi wa polisi, imebainika kuwa mbali na kosa la kughushi, watuhumiwa wote wanaandamwa na mashitaka mengine ya jinai ikiwemo ugaidi."

Kadhalika Msemaji wa Polisi ya Uganda amepuuzilia mbali madai kuwa watuhumiwa hao ni wakimbizi wa Kinyarwanda.

Maafisa wa polisi wa Uganda

Mawakili wa washukiwa hao hata hivyo wanasisitiza kuwa Wanyarwanda hao ni wakimbizi waliokuwa wakiishi katika kambi ya Nakivale wilayani Mbarara, na aghalabu yao ni wanawake na watoto wadogo. Aidha wamekosoa kitendo cha vyombo vya usalama kuwazuilia kwa muda zaidi ya ulioanishwa kwenye katiba pasina kuambiwa mashitaka yao.

Mawakili wa Wanyarwanda hao wamesisitiza kuwa, wateja wao walikamatwa wakielekea nchini Tanzania kushiriki Kongamano la Kikristo na kupekekwa katika kituo cha polisi cha Nalufenya, yapata kilomita 350 kutoka sehemu walikokamatwa.