Mursi aendelea kuandamwa na vifungo, ahukumiwa miaka mitatu mingine jela
Rais aliyeuzuliwa madarakani wa Misri, Muhammad Mursi amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa tuhuma za kuvivunjia heshima vyombo vya mahakama vya nchi hiyo.
Hukumu hiyo imetolewa leo dhidi ya Mursi ambaye hadi sasa anaendelea kuzuiliwa katika jela za nchi hiyo huku akiwa tayari amekwisha hukumiwa mara kadhaa kikiwemo kifungo cha maisha. Mbali na Muhammad Mursi, mahakama ya Misri pia imewahukumu watu 18 wengine kwa tuhuma hiyohiyo ya kuvivunjia heshima vyombo vya mahakama. Adha mahakama ya Misri imemtaka Mursi kulipa faini ya Pauni milioni moja za Misri kwa jaji Muhammad al-Nemr.
Hivi karibuni mahakama ya Misri ilitoa pendekezo kwa asasi za juu za kisheria la kutaka kufutwa uraia wa Mursi, waziri mkuu na waziri wa mambo ya ndani wa rais huyo wa zamani wa Misri. Tangu alipoondolewa madarakani rais huyo mwaka 2013, hadi sasa mamia ya wafuasi wake wamehukumiwa vifungo vya maisha au kunyongwa. Aidha tangu alipoondolewa madarakani rais huyo, Misri imekuwa ikikumbwa na wimbi la mashambulizi ya makundi ya kigaidi.