Watu wenye silaha wawashambulia Wakristo kusini mwa Nigeria, 14 wauawa
Polisi nchini Nigeria imetangaza kwamba, watu wenye silaha wamewashambulia kwa kuwapiga risasi Wakristo kusini mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na polisi ya nchi hiyo imesema kwamba, katika shambulizi hilo watu 14 wamepoteza maisha. Aidha imeongeza kwamba hujuma hiyo imetokea katika mji wa Port Harcourt, katikati ya jimbo la Rivers, kusini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Kadhalika polisi imetangaza kuanzisha uchunguzi mkali wenye lengo la kulitambua kundi lililohusika na shambulizi hilo la kigaidi, ingawa kidole cha awali cha lawama kimeelekezwa kwa makundi yanayogombania udhibiti wa vyanzo vya mafuta mjini hapo.
Jimbo la Rivers linajulikana kwa kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta ingawa wakazi wake wanaishi katika umasikini mkubwa. Makundi ya uhalifu yamekuwa yakitumia mashambulizi kwa lengo la kutaka kudhibiti vyanzo vya utajiri huo wa mafuta. Nigeria imekuwa ikishuhudia mashambulizi ya kila upande yanayotekelezwa na makundi kadhaa ya uhalifu suala ambalo limesababisha maelfu ya raia kuuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.