Wanasheria nchini Tanzania kuipandisha kizimbani serikali kwa kupiga marufuku maandamano
Jukwaa la Katiba nchini Tanzania (Jukata) linaloundwa na wanasheria limesema kuwa, litafungua kesi kuishitaki serikali wakati wowote kuanzia sasa kutokana na hatua yake ya kupiga marufuku maandamano ndani ya taifa hilo.
Kwa mujibu wa jukwaa hilo kesi hiyo itafunguliwa na Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (Leat), Dk Lugelemeza Nshala ambaye ataongoza jopo la mawakili 10 dhidi ya serikali. Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Jukata, Hebron Mwakagenda ambaye amebainisha kwamba tayari wamekusanya ushahidi wa kutosha wa kuishtaki serikali kwa hatua yake ya kuzuia maandamano ya amani nchini humo.
“Kikubwa katika mwaka huu ni kufungua kesi ya kupinga katazo la maandamano, maana ni kama yamefutwa kiaina hivi. Tumeshazungumza na wakili Dk Lugelemeza Nshala na amekubali kuongoza mawakili wengine 10 katika kesi hiyo.” Alisema Mwakagenda. Katazo la shughuli za kisiasa lilianza kutolewa na jeshi la polisi nchini Tanzania tarehe 6 Novemba, 2015 ambapo lilipiga marufuku maandamano na mikutano ya vyama vya siasa iliyokuwa imepangwa kufanyika kwa nyakati tofauti kwa madai ya kuwepo hali tete ya kisiasa nchini.
Aidha tarehe 23 Januari 2016, Rais John Pombe Magufuli wa nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki alitangaza kusimamisha shughuli za siasa ikiwemo mikutano na maandamano, alipokuwa akipokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wakati huo, Jaji Damian Lubuva. Hatua ya kupigwa marufuku shughuli za kisiasa imekuwa ikikosolewa na viongozi wa upinzani nchini Tanzania ambao wanasema kuwa mwenendo huo ni kuminya haki ya kujieleza.