Mawaziri 3 wapigwa kalamu nyekundu nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38515-mawaziri_3_wapigwa_kalamu_nyekundu_nchini_somalia
Waziri Mkuu wa Somalia, Hassan Ali Khaire amewafuta kazi mawaziri watatu katika nchi hiyo ambayo inakabiliana na mashambulizi ya kigaidi hususan kutoka kundi la kitakfiri la al-Shabaab.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 04, 2018 10:08 UTC
  • Mawaziri 3 wapigwa kalamu nyekundu nchini Somalia

Waziri Mkuu wa Somalia, Hassan Ali Khaire amewafuta kazi mawaziri watatu katika nchi hiyo ambayo inakabiliana na mashambulizi ya kigaidi hususan kutoka kundi la kitakfiri la al-Shabaab.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Habari ya nchi hiyo leo Alkhamisi imesema kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje, Yusuf Garaad Omar amefutwa kazi na nafasi yake kujazwa na Ahmed Ise Awad, huku mikoba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Abdi Farah Said Juha ikirithiwa na Mohamed Abdi Sabriye. 

Waziri Mkuu wa Somalia aidha amempiga kalamu Waziri wa Biashara na Leba, Khadra Ahmed Duale na kumteua Mohamed Abdi Hayir kujaza nafasi yake.

Taarifa ya Wizara ya Habari ya Somalia imesema kulikuwa na udharura mkubwa wa kujaza nafasi hizo ili mawaziri hao wapya waipige jeki serikali kutimiza malengo na kumaliza mrundiko wa kazi unaoikabili. 

Rais Abdullah Mohammed Farmajo wa Somalia

Mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka uliomalizika, Waziri Mkuu wa Somalia alimfuta kazi, Iman Abdullahi Ali aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Dini wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika; na kabla ya hapo aliwafuta kazi Waziri wa Ulinzi na Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo na kujaza nafasi zao mara moja.

Kwa miongo mitatu sasa Somalia ambayo imekuwa ikiendeshwa bila ya serikali kuu yenye nguvu imekuwa ikishuhudia fujo, mauaji na mashambulizi ya kila namna.