Uhusiano wa Sudan na Misri wazidi kuharibika; Khartoum yamwita nyumbani balozi wake
Uhusiano wa Sudan na Misri umezidi kuharibika baada ya serikali ya Khartoum kumwita nyumbani balozi wake aliyeko Cairo Misri.
Qaribullah Al-Kheder, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan amesema kuwa, Khartoum imemwita nyumbani balozi wake wa Cairo Misri kwa ajili ya mashauriano zaidi.
Msemaji wa serikali ya Sudan hakuwa tayari kutoa ufananuzi zaidi ghairi ya kusisitiza kwamba, serikali ya Khartoum imemwita nyumbani Abdel-Mahmoud Abdel Halim balozi wake aliyeko Cairo Misri kwa ajili ya mashauriano.
Duru za karibu na serikali ya Khartoum zinasema kuwa, hatua hiyo imechukuliwa baada ya kushadidi mvutano na mzozo baina ya nchi mbili hizo kuhusiana na eneo la Pembe Tatu la Hala'ib (Hala'ib Triangle) linalogombaniwa na nchi mbili hizo.
Baadhi ya duru zinaamini kuwa, safari ya Rais Recep Tayyip Erdogan nchini Sudan imeshadidisha vita vya maneno baina ya viongozi wa Khartoum na Cairo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan alifuta safari yake ya kuitembelea Misri ambapo ilipangwa kuwa akutane na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Misri Sameh Shoukry na kuunda kamati ya mashauriano ya kisiasa juu ya uhusiano wa pande mbili pamoja na masuala ya kieneo.