Kufutwa kazi mawaziri watatu nchini Somalia
-
Waziri Mkuu wa Somalia, Hassan Ali Khayre
Waziri Mkuu wa Somalia amewafuta kazi mawaziri wa mambo ya nje, wa mambo ya ndani na wa biashara wa nchi hiyo na kuteuwa watu wengine kushika nafasi hizo.
Waziri Mkuu wa Somalia, Hassan Ali Khayre amewafuta kazi Yusuf Garaad Omar, waziri wa mambo ya nje, Abdi Farah Saeed Haja, waziri wa mambo ya ndani na Khadhrat Ahmed Wali, waziri wa biashara wa nchi hiyo na nafasi zao kuchukuliwa na watu wengine wapya.
Licha ya kupita karibu mwaka mmoja tangu ulipofanyika uchaguzi mkuu nchini Somalia na licha ya ahadi kemkem zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi hususan katika suala la kupambana na ugaidi na kurejesha amani na utulivu nchini humo, lakini hali ya kisiasa na kiuchumi ni mbaya huku mashambulizi ya kigaidi yakiendelea katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, bali hata yameongezeka zaidi ikilinganishwa na huko nyuma. Mripuko mkubwa wa kigaidi uliotokea hivi karibuni mjini Mogadishu uliua zaidi ya watu 500.
Kuendelea mashambulizi ya kigaidi kumeitumbukiza serikali ya Somalia katika wimbi kubwa la lawama za kufeli mipango yake ya kupunguza mashambulizi ya genge la kigaidi la al Shabab. Ukosefu huo wa usalama umeathiri moja kwa moja masuala ya kiuchumi na kusababisha mgogoro wa kimaisha kwa wananchi wa Somalia. Kwa upande mmoja ukata, umaskini na ukosefu wa kazi umeongezeka na katika upande wa pili, ukame na kukosekana mahitaji ya lazima ya chakula umekuwa ni mzigo mkubwa kwa wakazi wa maeneo mengi ya Somalia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema: Kundi la al Shabab na magenge mengine yenye silaha yanayoipinga serikali yamekuwa yakishambulia shehena za misaada ya kibinadamu inayotumwa nchini humo. Hali hiyo imekwamisha juhudi za kuwafikisha misaada wakimbilizi milioni mbili wa Somalia.
Hali hiyo inashuhudiwa katika hali ambayo nchi za Magharibi na hususan Marekani bado zinaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo kwa madai ya kupambana na ugaidi. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, Marekani ambayo ndiyo iliyoweka misingi na kuunda magenge ya kigaidi na yenye misimamo mikali kama Daesh (ISIS) al Qaida na Taleban, ilisubiri magenge hayo yapate nguvu kidogo baada ya kuyaunda na kuyapa silaha, halafu ikatokea mlango wa pili na kudai kupambnaa nayo na kwa njia hiyo imeweza kuimarisha uwepo wake wa kijeshi katika nchi za Waislamu kwa hila zake hizo za kishetani. Marekani inajifanya kupambana na magaidi, lakini kimsingi si wakweli hata kidogo katika vita vyao dhidi ya ugaidi. Marekani na waitifaki wake kwa upande mmoja wanajifanya kupambana na magenge ya kigaidi ambayo ni wao wenyewe waliyoyaunda na kuyapa silaha na baadaye kuyafungulia njia ya kuingia katika nchi za Kiislamu na wakati huo huo wanaendelea kuyaunga mkono kisiasa, kifedha kisilaha na kimafunzo kupitia imma kubadilisha tu majina yao au kutoyashambulia kwa nguvu za kuweza kuyaangamiza na kuyafuta kabisa katika uso wa dunia. Wachambuzi hao wanasema, vita visivyoisha vya karibu miaka 20 sasa vya nchini Afghanistan ni ushahidi wa wazi wa uhakika huo. Hali ya Somalia nayo haiko mbali na uhakika huo na swali linaloulizwa na weledi wa mambo ni hilo hilo linaloulizwa kuhusu magenge mengine ya kigaidi yanayofanya jinai katika nchi nyingine duniani kwamba yanapata wapi silaha, maeneo na fedha za kuendeleshea jinai zao kama si kutoka katika nchi hizo hizo za Magharibi, wazalishaji wakuu wa silaha ulimwenguni?

Kwa upande wake, kundi linalopinga vita linalojulikana kwa jina la "Kituo cha Hatua za Kimataifa" lenye makao yake nchini Marekani limesema: Stratijia ya kijeshi ya Marekani barani Afrika haina uhusiano wowote na vita dhidi ya ugaidi kwani Washington lengo lake ni kupora utajiri wa maliasili wa nchi za Afrika na kudhibiti masoko ya kiuchumi ya bara hilo. Siasa hizo zimejengwa juu ya msingi wa kulinda maslahi ya Marekani na hilo ndilo lengo la kutumwa na kuongezwa idadi ya wanajeshi wa Marekani, barani Afrika. Somalia katika hili iko kwenye nafasi nzuri sana ya kiistratijia ya kuweza kufanikisha malengo hayo ya Marekani.
Tukirejea katika mabadiliko mapya ndani ya serikali ya Somalia ni kwamba ingawa kufutwa kazi mawaziri hao watatu kumefanyika kwa shabaha ya kurejesha utulivu na amani nchini humo, lakini inavyoonekana ni kwamba amani na utulivu wa nchi hiyo unategemea kuweko serikali yenye nguvu, madubuti ambayo itaweza kukata uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Somalia.