Upinzani Gabon wapinga kuondolewa kikomo cha mihula ya urais
Vyama vya upinzani nchini Gabon vimepinga vikali hatua ya Bunge la nchi hiyo ya kuifanyia marekebisho katiba, kwa lengo la kumuondolea visiki njiani Rais Ali Bongo wa nchi hiyo ili aendelea kung'ang'ania madaraka.
Kiongozi wa upinzani katika nchi hiyo ndogo yenye utajiri wa mafuta na madini, Jean Ping ameyataja mabadiliko hayo kama njia za kidikteta zinazokiuka misingi ya utawala na mamlaka.
Wabunge nchini Gabon Jumatano iliyopita walipiga kura kuunga mkono mabadiliko hayo ya katiba, yanayoidhinisha suala la kuondolewa kikomo cha mihula miwili ya miaka saba kwa rais.
Mbali na kipengee cha kumruhusu rais kuendelea kuhudumu kwa zaidi ya mihula miwili, lakini pia kipengee kingine cha marekebisho hayo kinasema rais huyo hawezi kufunguliwa mashitaka baada ya kuondoka madarakani.
Ali Bongo alishinda uchaguzi wa rais wa Agosti mwaka 2016 kwa kupata asimilia 50 ya kura huku mpinzani wake ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jean Ping akipata asilimia 47.
Ping hata hivyo alikataa kutambua rasmi matokeo ya uchaguzi huo yaliyompa ushindi mpinzani wake.