Somalia yaitaka jamii ya kimataifa isaidie mchakato wa mageuzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39061-somalia_yaitaka_jamii_ya_kimataifa_isaidie_mchakato_wa_mageuzi
Waziri Mkuu wa Somalia Bw. Hassan Ali Khaire ametoa wito kwa jamii ya kimataifa iunge mkono serikali ya Somalia kuanzisha mchakato wa mageuzi kwa idara za usalama za nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 16, 2018 11:11 UTC
  • Somalia yaitaka jamii ya kimataifa isaidie mchakato wa mageuzi

Waziri Mkuu wa Somalia Bw. Hassan Ali Khaire ametoa wito kwa jamii ya kimataifa iunge mkono serikali ya Somalia kuanzisha mchakato wa mageuzi kwa idara za usalama za nchi hiyo.

Khaire ambaye Jumatatu alisimamia mkutano wa mageuzi ya idara za usalama mjini Mogadishu, amesema Somalia bado inahitaji tume ya ulinzi wa amani ya Umoja wa Afrika AMISOM kusaidia kulinda utulivu.

AMISOM imeahidi kuendelea kuunga mkono mchakato wa mpito kwenye majukumu muhimu, zikiwemo kulinda barabara muhimu, kulinda usalama wa maeneo yenye watu wengi, na kutoa mafunzo na misaada kwa idara za usalama za Somalia zikiwemo jeshi na polisi, kwa kushirikiana na tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia na kuendana na mipango ya usalama ya kitaifa.

Umoja wa Afrika umetuma kikosi chake katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Kikosi hicho cha AMISOM kina wanajeshi kutoka Uganda, Kenya, Burundi na Ethiopia. Askari zaidi ya 22 elfu wanaunda kikosi hicho cha AU kwa ajili ya kupambana na kundi la al Shabab huko Somalia.

Ingawa kundi la al Shabab limefurushwa katika miji yote mikubwa na maeneo muhimu ya Somalia, lakini bado lina wanamgambo wake katika baadhi ya vijiji na miji na hufanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia na maafisa wa Serikali.