Umoja wa Mataifa watahadharisha tena kuhusu ukame Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39167-umoja_wa_mataifa_watahadharisha_tena_kuhusu_ukame_somalia
Umoja wa Mataifa umetahadharisha tena kuhusiana na ukame katika nchi ya pembe ya Afrika ya Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 19, 2018 01:06 UTC
  • Umoja wa Mataifa watahadharisha tena kuhusu ukame Somalia

Umoja wa Mataifa umetahadharisha tena kuhusiana na ukame katika nchi ya pembe ya Afrika ya Somalia.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeonya juu ya Somalia kukumbwa tena na ukame na hivyo kuifanya hali ya kibinadamu ya nchi hiyo kuwa mbaya zaidi.

Vyombo vya habari vimemnukuu Vincent Lelei, Naibu Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia akisema kuwa, mamilioni ya raia wa nchi hiyo wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na machafuko na ukame.

Aidha amesema kuwa, mamia ya watoto wa Somalia wanakabiliwa na hali mbaya ya lishe duni.

Wanamgambo wa al-Shabab wa Somalia

Naibu Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia ameongeza kuwa, katika mwaka uliopita wa 2017, Umoja wa Mataifa ulifanikiwa kukabiliana na ukame katika nchi hiyo. Amesema ili hatua za kukabiliana na ukame ziweze kufanikiwa mwaka huu huko Somalia kunahitajika kiwango cha dola bilioni moja na milioni 600. 

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, kwa kuzingatia uhaba wa chakula unaoikabili nchi hiyo kwa sasa, wananchi wengi wanahitajia misaada ya haraka ya chakula.

Mbali na majanga hayo ya kimaumbile, Somalia inakabiliwa pia  na harakati za kundi la kigaidi la al-Shabaab ambalo limekuwa likifanya mashambulizi ya kigaidi nchini humo.