Jan 21, 2018 07:43 UTC
  • Chama tawala Afrika Kusini kumuuzulu Rais Zuma kwa nguvu

Chama tawala nchini Afrika Kusini ANC kimetishia kumuuzulu Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo iwapo hatakubali kuachia ngazi kwa khiari.

Wanachama wa Kamati Kuu Taifa ya ANC walikutana jana Jumamosi, ambapo duru zinasema kuwa waliainisha mkakati na mbinu watakazotumia kumshinikiza Zuma aachie madaraka.

Hata hivyo msemaji wa chama hicho amekataa kuthibitisha au kukanusha ripoti hizo alipotakiwa kufanya hivyo na waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya eNCA, taasisi sita zenye ushawishi mkubwa za chama hicho tawala zimekubaliana kwa kauli moja kuwa, iwapo Zuma atakaa kujiuzulu kwa khiari, basi hawatakuwa na budi kumuuzulu.

Maandamano dhidi ya Zuma mjini Johannesburg

Wanachama wa ANC katika miezi ya hivi karibuni wamekuwa wakimtaka Zuma ajiuzulu kufuatia msururu wa kashfa za ufisadi zinazomkabili.

Mbali na mashinikizo ya chama tawala, lakini pia vyama vya upinzani na wananchi wa Afrika Kusini wamekuwa wakifanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi wakitaka kiongozi huyo ajiuzulu, hatua ambayo hadi sasa imeshindwa kuzaa matunda.

Tags