Wanasiasa Misri watoa wito wa kususiwa uchaguzi wa rais
Wanasiasa wa kambi ya upinzani nchini Misri wamewataka wananchi wa nchi hiyo kususia uchaguzi ujao wa rais.
Vinara kadhaa wa kambi ya upinzani wa Misri wametoa taarifa wakiwataka wananchi wa nchi hiyo kususia uchaguzi wa rais ili kuonesha upinzani wao dhidi ya mienendo na sera za rais wa sasa wa nchi hiyo, Abdel Fattah al Sisi dhidi ya wapinzani wa serikali.
Abdel Moneim Aboul Fotouh, Hisham Genena na Muhammad Anwar Sadat ni miongoni mwa wanasiasa wa Misri waliotoa taarifa wakitaka kususiwa uchaguzi ujao wa rais. Taarifa hiyo imetolewa siku moja baada ya askari usalama kumshambulia Hisham Genena akiwa mbele ya nyumba yake mjini Cairo na kumjeruhi.
Wakili wa mwanasiasa huyo anasema shambulizi hilo lilikuwa jitihada za serikali ya al Sisi za kutaka kumteka nyara mwanasiasa huyo wa upinzani.
Wagombea kadhaa wa vyama vya siasa vya upinzani wamejiengua katika kinyang'anyiro cha kugombea kiti cha rais wakilalamikia mashinikizo na ukandamizaji unaofanywa na vyombo vya dola. Mwenendo huu unaufanya uchaguzi huo kuwa na mgombea mmoja wa kiti cha rais.
Uchaguzi wa rais wa Misri umepangwa kufanyika tarehe 26 hadi 28 za mwezi Machi mwaka huu.