Algeria yatahadharisha kuhusu kurejea magaidi barani Afrika
Waziri Mkuu wa Algeria ametahadharisha kuhusiana na hatari ya kurejea barani Afrika wanachama wa makundi ya kigaidi wakiwemo wa kundi la wakufurishaji la Daesh.
Ahmed Ouyahia amesema hayo katika hotuba yake kwenye mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika huko Addis Ababa Ethiopia na kusisitiza kwamba, nchi za bara hilo zinapaswa kuwa makini na suala la kurejea barani humo wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh.
Waziri Mkuu wa Algeria ameongeza kuwa, kushindwa kundi la kigaidi la Daesh huko Syria na Iraq ni mafanikio makubwa katika vita vya kupambana kila upande na ugaidi.
Hata hivyo ametahadharisha kwamba, vita dhidi ya ugaidi vina malengo mbalimbali na moja ya mambo ambayo yanapaswa kuchungwa ni suala la kurejea katika nchi zao wanachama wa makundi ya kigaidi waliokuwa huko Syria na Iraq.
Viongozi wa Umoja wa Afrika wamekuwa wakitahadharisha kwamba, kuna uwezekano wa kurejea barani Afrika wanachama zaidi ya elfu sita wa kundi la kigaidi la Daesh.
Umoja wa Afrika unasema kuwa, kurejea kwa wanachama hao wa Daesh katika nchi zao huko Afrika ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa nchi hizo.
Hivi karibuni gazeti la The Sun la Uingereza liliripoti kwamba, kuna uwezekano Abubakar al Baghdadi, kiongozi wa kundi la kigaidi la Daesh akawa amekimbilia katika nchi ya Afrika ya Chad au katika eneo moja jirani na Niger.