Wapinzani wa serikali ya Burundi wakutana kuunganisha nguvu zao
Wapinzani wa serikali ya Burundi walioko nje ya nchi wameanzisha jitihada za kuunda kambi na muungano dhidi ya serikali ya Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo.
Ripoti zinasema kuwa, viongozi wa kambi ya upinzani dhidi ya serikari ya Burundi wamekutana katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi wakitaka kuwepo msimamo mmoja dhidi ya maamuzi ya serikali ya Bujumbura hususan kupinga kura ya maoni ya katiba ambayo wanasema itaanda mazingira ya kubakia zaidi madarakani Rais Pierre Nkurunzinza.
Wapinzani hao wamechukua uamuzi wa kuilazimisha serikali ya Bujumbura kuketi kwenye meza ya mazungumzo. Washiriki katika mkutano huo pia wameutaka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Afrika Kusini na nchi za kanda ya mashariki mwa Afrika ambao ni wadhamini wa makubaliano ya Arusha kuzuia kura ya maoni ya marekebisho ya katiba nchini Burundi.
Wamesisitiza kuwa kura hiyo ya maoni itakuwa mwisho wa makubaliano ya amani ya Arusha yaliyotiwa saini mwaka 2000 ambayo yalihitimisha vita vya ndani vilivyosababisha vifo vya watu laki tatu nchini Burundi.
Burundi ilitumbukia katika machafuko mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mara ya tatu mfululizo.