Sudan Kusini yamuita nyumbani balozi wake kutoka Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39919-sudan_kusini_yamuita_nyumbani_balozi_wake_kutoka_marekani
Sudan Kusini imemuita nyumbani balozi wake wa Marekani, huku mzozo kati ya Washington na Juba kuhusu kuwekewa vikwazo vya silaha nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ukipamba moto.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 05, 2018 01:07 UTC
  • Sudan Kusini yamuita nyumbani balozi wake kutoka Marekani

Sudan Kusini imemuita nyumbani balozi wake wa Marekani, huku mzozo kati ya Washington na Juba kuhusu kuwekewa vikwazo vya silaha nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ukipamba moto.

Ateny Wek Ateny, Katibu wa Rais Salva Kiir wa nchi hiyo katika masuala ya vyombo vya habari amenukuliwa akisema kuwa, serikali ya Juba imemuita nyumbani Garang Diing Akuong kwa mashauriano, hususan baada ya Washington kuiwekea nchi hiyo ya Afrika vikwazo vya silaha.

Kadhalika Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Kusini imethibitisha habari hiyo ya kuitwa nyumbani balozi, siku mbili baada ya Marekani kupiga marufuku kuuziwa silaha serikali ya nchi hiyo ndogo ya Afrika, eti kwa kushindwa kumaliza mapigano ndai ya nchi. 

Mwishoni mwa mwaka 2016 baada ya Washington kutangaza vikwazo vipya dhidi ya Sudan Kusini, Makamu wa Rais wa nchi hiyo ya Kiafrika, Taban Deng Gai aliilaumu Marekani kwa siasa zake zisizo sahihi kuhusiana na nchi hiyo na kusema kuwa, Juba inahitajia misaada ya kila namna na si vikwazo.

Jeshi la Sudan Kusini

Hii ni katika hali ambayo, vyombo vya habari nchini humo vimewahi kuripoti kuwa, Shirika Kuu la Kijasusi la Marekani (CIA) linaunga mkono na kulizatiti kwa silaha kundi jipya la waasi linaloongozwa na aliyekuwa Naibu Mkuu wa Jeshi katika nchi hiyo, Jenerali Thomas Cirilo Swaka.

Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013, miaka miwili tu baada ya kujitenga na jamhuri ya Sudan, baada ya Rais Salva Kiir kuhitalifiana na makamu wake Riek Machar.