Watu kadhaa wauawa katika maandamano nchini Guinea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i40303-watu_kadhaa_wauawa_katika_maandamano_nchini_guinea
Kwa akali watu wawili wamethibitishwa kupoteza maisha katika ghasia zilizotokana na maandamano yaliyofanyika jana Jumatatu nchini Guinea Conakry.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 13, 2018 04:01 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika maandamano nchini Guinea

Kwa akali watu wawili wamethibitishwa kupoteza maisha katika ghasia zilizotokana na maandamano yaliyofanyika jana Jumatatu nchini Guinea Conakry.

Albert Damantang Camara, msemaji wa serikali amethibitisha habari ya kutokea vifo hivyo ingawaje anasisitiza kuwa, vimetokea katika mazingira ya kutatanisha.

Hata hivyo duru za kiusalama zinaarifu kuwa, watu hao waliuawa na maafisa wa polisi, katika wilaya ya Hamdallaye, moja ya ngome za upinzani viungani mwa mji mkuu, Conakry.

Maandamano ya jana kwa upande mmoja yalikuwa ya kulalamikia matokeo ya uchaguzi wa mitaa uliofanyika Fenruari 4, huku walimu pia wakiandamana kushinikiza kuboreshwa kwa mazingira ya kazi kwa upande mwingine.

Maandamano ya wapinzani katika mji mkuu Conakry

Maandamano ya jana yamefanyika chini ya wiki moja baada ya watu 50 kutiwa mbaroni kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya watoto watano katika ghasia za baada ya uchaguzi huo wa serikali za mitaa.

Takriban watu 10 wanaripotiwa kuuawa hadi sasa katika machafuko ya baada ya uchaguzi huo, mbali na wengine wengi kujeruhiwa na makumi kutiwa nguvuni.