Serikali yavunja chama kikuu cha upinzani Equatorial Guinea
Mahakama moja ya Equatorial Guinea imevunja chama kikuu cha upinzani nchini humo sambamba na kuwasweka jela makumi ya wanaharakati.
Kanali ya televisheni ya serikali TVGE, imemnukuu Jaji Jose Rafael Nguema wa Mahakama ya Mongomo akisema kuwa, chama hicho cha Citizens for Innovation (CI) kitaondolewa kwenye sajili ya vyama vya siasa nchini humo mara moja.
Naibu Mwendesha Mashtaka Mkuu wa serikali, Anatalio Nzang amesema chama hicho kimevunjwa kwa kuhatarisha usalama wa taifa.
Aidha katika hukumu hiyo iliyotolewa jana, korti hiyo imewahukumu kifungo cha miaka 30 jela wanaharakati 21 wa chama hicho, kwa kile kinachosemekana ni kupatikana na hatia ya uhaini.
Mwishoni mwa mwaka uliopita, maafisa usalama walivamia majengo ya ofisi za chama hicho katika miji ya Malabo na Bata, miji mikuu ya kisiasa na kiuchumi ya nchi hiyo na kuwatia mbaroni makumi ya wafuasi wa chama hicho, muda mfupi baada ya kufanyika uchaguzi mkuu katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Disemba 24 mwaka jana na baada ya kutibuka kwa jaribio hilo la mapinduzi dhidi ya serikali, polisi walivamia majengo ya ofisi za chama hicho na kuwakamata wanaharakati 141.
Nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika imekuwa ikiongozwa na Rais Teodoro Obiang Nguema tangu mwaka 1979.