Algeria kuendelea kuiunga mkono serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria
Waziri Mkuu wa Algeria amesema kuwa, nchi yake itaendelea kuiunga mkono serikali halali iliyochaguliwa na wananchi ya Rais Bashar al Assad wa Syria.
Televisheni ya al Alam imemnukuu Abdelmalek Sellal akisema hayo leo wakati alipoonana na Walid Muallem, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria mjini Algiers na kusisitiza kuwa, uungaji mkono wa nchi yake kwa serikali ya Damascus utaendelea na kwamba Algeria haitaacha kuwa pamoja na Syria katika mazingira yote.
Abdelmalek Sellal ameeleza matumaini yake kuwa, hali ya usalama na utulivu itarejea kama zamani nchini Syria.
Aidha Wazri Mkuu wa Algeria amezilaumu nchi za Kiarabu kwa kushindwa kushughulikia masuala makuu na ya asili yanayouhusu ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu hususan kadhia ya Palestina.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ameishukuru Algeria kwa msimamo wake huo na kuzungumza na Waziri Mkuu wa nchi hiyo kuhusu masuala mbalimbali kama vile mazungumzo baina ya Wasyria wenyewe kwa wenyewe, ushindi mtawaliwa linaopata jeshi la Syria katika mapambano dhidi ya genge la kigaidi la Daesh (ISIS) na hasa kufanikiwa jeshi hilo kuukomboa mji wa kihistoria wa Tadmor (Palmyra).
Walid Muallem aliwasili nchini Algeria jana Jumanne kwa ajili ya kufanya ziara rasmi ya siku tatu akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa nchi yake kama vile Faisal Mekdad, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria. Ziara hiyo imefanyika kwa mwaliko wa Ramtane Lamamra, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria.