LHRC yaitaka Tume ya Uchaguzi Tanzania kusikiliza malalamiko ya wadau
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania (LHRC), kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo (NEC) kufanyia kazi changamoto na malalamiko yaliyoibuliwa na wadau wakati na baada ya uchaguzi mdogo wa ubunge Kinondoni na Siha.
Taarifa iliyotolewa na Naemy Sillayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, imesema kuwa, NEC inatakiwa kuzifanyia kazi changamoto hizo bila kujali udhaifu na namna ya uwasilishaji wake. Kwa mujibu wa kituo hicho, kuibuliwa kwa changamoto hizo kunalenga kujenga jamii yenye haki na usawa ndani ya Tanzania na si vinginevyo.
Sillayo ameyasema hayo leo alipokuwa akijibu hoja zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo (NEC) wiki iliyopita kutokana na tamko lililotolewa na Umoja wa Asasi za Kiraia (AZAKI) nchini humo ambapo zilikosoa mwenendo wa uchaguzi na matukio mbalimbali yanayojiri ndani ya taifa hilo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kadhalika Naemy Sillayo amesema kuwa, LHRC inakubaliana na hoja zilizotolewa na AZAKI za kutaka NEC kuboresha kanuni za usimamizi wa uchaguzi na kutovibana vyombo vya habari. Asasi mbalimbali nchini Tanzania zimekuwa zikilalamikia matukio ya kisiasa, mauaji na utekaji nyara wa watu ambayo yamekuwa yakishuhudiwa katika siku za hivi karibuni huku zikiitaka serikali ya Dar es Salaam kuchukua hatua kali kudhibiti hali hiyo.
Kuhusiana na suala hilo hivi karibuni pia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe alilituhumu jeshi la polisi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) kuwa imekuwa na miamala mibaya dhidi ya upinzani nchini humo. Umoja wa Ulaya (EU) pia ulitoa tamko kuhusiana na matukio ya utekaji nyara na mauaji ambayo yamekuwa yakitokea nchini Tanzania na kuitaka serikali ya Dar es Salaam kufanya uchunguzi wa kina juu ya matukio hayo.